MTUNZI : GEOFREY MALWA
“Mke wangu ananipenda sana,” Tasriki alisema hivyo
“Kitu pekee ambacho unatakiwa ukiamini ni kuwa wewe unampenda mkeo, unaujua ukweli wa moyo wako tu na sio wa mtu mwingine,” Jose alimjibu
“Ananijali, ananiheshimu, kila muda haachi kunijulia hali, anawapenda ndugu zangu, kweli kaka unataka kuniambia itafika siku anisaliti?”
“Nakukumbusha tu kuwa, ukianza kuwaza kuwa mkeo hawezi kukusaliti ujue umeanza kufikiria kwa kuongozwa na hisia,”
“Yaani nyumbani kwangu napaona kama mbinguni, kwanza mzuri, sijawahi kumchoka, vingine mpaka nasita kuvitangaza, Mungu amuweke hai mke wangu,’
“Mimi pia nakuombea sana ndugu yangu ila nikushauri kitu,”
“Niambie,”
“Mkeo sio malaika, naye hukosea kumbuka hilo, pia mkeo kabla ya wewe alikuwa na watu wengine, kikubwa ni kuvumiliana na kujazia pale alipopungua mwenzio,”
“Nashukuru sana ndugu yangu,”
“Sawa, na kwanini umeamua kufikiria hivyo?”
“Naona ndoa nyingi zinavunjika kwasababu ya usaliti,”
“Hilo likufunze jambo lakini zipo zinazodumu na hawasalitiani,”
“Kama mimi,”
“Yaani unavyojiamini, naomba Mungu iwe hivyo,”
“Sasa unafikiri mke wangu anaweza akapumuliwa na mwanaume mwingine?”
“Siwezi kusema anaweza, ila usiseme hawezi, hii dunia haina mbingu mpaka wapatikane watu waliokamilika,”
“Ila ndugu yangu inabidi uoe, uchague mwanamke mzuri kama shemeji yako, utafurahia maisha, kwanza huyo ananipigia,”
“Hello kipenzi cha moyo wangu,”
“Mume wangu nimekumisi sana, kazi zinaendaje?”
“Salama kabisa, sijui wewe unaendeleaje na hali,”
“Niko salama kabisa,”
“Nakupenda mno,”
“Hunishindi mimi…”
Baada ya Tasriki kuzungumza na mkewe, alianza kuelezea jinsi alivyo na furaha na mkewe, Jose alimuunga mkono huku akimuonea huruma siku yakimkuta mambo.
Tasriki na Jose walikuwa ni marafiki waliokutanishwa na kazi zao, wote wawili walikuwa wakimiliki maduka makubwa ya ‘Spea’ za magari na pikipiki. Walikuwa wakishauriana mambo mengi japo Jose bado alikuwa hajaoa.
Tukirudi huku upande wa mke wa Tasriki aliyeitwa Nana, ni kweli alikuwa mzuri sana, mzuri na alishawishi kweli, ungweza kumshangaa jinsi Tasriki alivyo na furaha lakini ukimtazama mkewe utagundua sababu ya kujivunia alikuwa nayo.
..
Nana alikuwa ni mrefu, rangi ya maji ya kunde, dimpo kwa mbali zilichungulia, alivutia usoni mpaka umbo lake, moja kati ya vitu alivyokuwa akizingatia ni mlo kamili tena ule unaolenga kulinda mwili wake, alijijua kuwa ana umbo zuri na hakuhitaji liharibike.
Siku hiyo akiwa nyumbani alipokea simu kutoka kwa rafiki yake aliyeitwa Spora, walisalimiana kama kawaida na kupeana umbea mdogo mdogo ambao hupeana kila wakiongea, Spora ndiye aliyekuwa rafiki mkubwa sana wa Nana, alizijua siri zake nyingi sana tangu wakiwa sekondari, mpaka chuo walisoma kimoja, ni marafiki walioshibana mno,
“Sasa shosti yangu kuna taarifa imekuja hapa, Travo anaumwa tunaenda kumuona, utaenda?”
“Hivi kwa alivyonifanyia bado niwe na moyo wa kumuona?”
“Unanisindikiza tu, tunakwenda na shemeji yako,”
“Na mume wangu nimwachie nani?”
“Kwani hospitari tunatumia dakika ngapi? Mimi pia nina kazi zangu, tunakwenda kumuona saa kumi kamili, tunakaa pale dakika tano tu,”
“Unaenda na gari?”
“Ndiyo, na tutakurudisha mpaka nyumbani,”
“Sawa ila sitoingia huko ndani,”
“Sawa.”
Basi Nana alijiandaa kisha akapitiwa na gari la kina Spora aliyekuwa na mume wake. Mpaka hospitari walifika, Nana alibaki nje ya chumba cha wodi aliyolazwa Travo.
Nana kumbukumbu zilimtesa sana, alikumbuka siku moja alivyokuwa amelazwa, mtu pekee aliyekuwa pembeni yake ni Travo, alimhudumia mpaka alipopata nafuu na kurudi naye nyumbani, aliyakumbuka hayo na kujawa na moyo wa huruma, alipoanza kupiga hatua za taratibu kuuelekea mlango wa wodi, alimuona mwanamke ambaye ndiye alimfumania na Travo kipindi hicho wako chuo,
“Afadhari nimekuona, najua utakuwa na hasira feki sana na mimi,”
“Hasira feki! Kwanza sasahivi nina ndoa yangu, sijali tena, endeleeni tu,”
“Masikini! Ukiujua ukweli, sasahivi utakwenda kumpigia magoti yule mwanaume,”
“Ukweli gani?”
“Siku ile nilitumwa kuja kuvuruga mapenzi yenu, hakuna hata tulichofanya na Travo, sikuwa na hela kumalizia kulipa ada, Doni ndiye aliusuka mpango wote mwanzo mpaka mwisho,”
“Unasemaje?”
“Hivyo ndivyo ilivyokuwa, mazingira yote yalitengenezwa, kuanzia jumbe kwenye simu yake, na barua pepe zake, zote tulitengeneza, Doni alikuwa anakupenda sana lakini ndio hivyo hakukupata
..
MWISHO