Search This Blog

Sunday, July 24, 2022

LOVE AND LAW

  

MTUNZI : GEOFREY MALWA



Katika kijiji cha Koikoi,wilaya ya Umba,mkoa wa Sengeni nchini Bambai,palikuwa na kijana mmoja aliyeitwa Dennis.Miaka ishirini na tano ndio ulikuwa umri wake.Urefu wa wastani,rangi nyeusi iliyong’aa,mwili wa mazoezi,hizo ndizo zilikuwa sifa zilizowavutia wasichana wengi katika kijiji cha koikoi kilichokua karibu sana na wilayani.

Wanakoikoi wengi walijishughulisha na kilimo,biashara ndogondogo,huku wengine waliobahatika kugundua vipaji vyao walivitumia vizuri.Dennis alikuwa ni kijana mmojawapo kati ya wenye vipaji aliyekigundua na kukitumia kwa ajili ya kujipatia kipato.Kipaji cha kuchonga vinyago na kuchora picha ndicho alijaaliwa na dalili zilionekana tangu akiwa mdogo.

Dennis aliweza kutengeneza vinyago na kuchora picha nzuri za kuvutia ambazo aliuza ndani na nje ya nchi.Watalii pia walikuwa ni wateja wake wakubwa.Kazi yake ilitangazika sana,hali iliyosababisha soko lake kupanuka kila kukicha.Kazi hiyo iliyafanya maisha yake kuwa mazuri,alikuwa ni miongoni mwa vijana wadogo waliomiliki aina ya pesa iliyoridhisha.

Wakati huo Dennis akiwika na kipaji chake,Serikali ya nchi ya Bambai ilikuwa ikisumbuliwa sana na matukio ya uhalifu yaliyokuwa yakiendelea.Jeshi la polisi lilionekana halijavaa viatu vyake ipasavyo kwasababu lilielemewa na matukio hayo ya uhalifu yaliyokuwa yakizuka kila wakati.Habari magazetini zilizagaa kuonyesha sura za watu waliotafutwa na polisi ili kama wakionekana mahali popote raia mwema atoe taarifa kusaidia kupunguza vitendo hivyo.

***

Watu wengi hususani siku za sikukuu,walifurika kwenye duka la Dennis kwa ajili kuangalia Picha mbalimbali na vinyago kisha kupiga navyo picha.Nakumbuka ilikuwa ni Tarehe moja mwezi kwanza mwaka 2012,kama kawaida watu walisheheni dukani kwa Dennis wakifurahia mwaka huo mpya wa 2012.Moja kati ya familia iliyohudhuria siku hiyo dukani mwa Dennis ilisikika ikizungumza hivi,
“nimefurahi sana mume wangu leo,kumbe ndani ya hili duka ndio kuzuri hivi?” mke alimwambia mumewe
“ninachojali ni furaha yako na mwanangu,ninyi mkifurahi mimi ni mara mbili yake,” alijibu mume akiachia tabasamu la upendo
“baba naomba nikapige picha na simba,”

...


mtoto wao aliyeitwa Lisa aliongea hivyo kwa kudeka
“ulitakalo limeshakuwa mwanangu,twende.” Baba alimbeba mwanaye Lisa kisha wakaenda kupiga picha na kinyago hicho cha Simba.

Baba wa familia hiyo aliitwa Leonard Kamosa,alikuwa ni Afisa mpelelezi aliyetegemewa hasa.Aliipenda sana familia yake na kuipa kipaumbele kila wakati.Lisa alilelewa katika mazingira ya upendo ambayo si watoto wengi waliobahatika kama yeye kulelewa katika mazingira hayo.

Katika utani wa mapenzi,mama Lisa alimtania mumewe kwa kujifananisha na moja kati ya kinyago cha msichana kilichochongwa vizuri ambacho kwa muda huo vijana wengi walikizunguka wakikiangalia, “hapana mke wangu,bado sijafikia hatua ya kukufananisha na kinyago nisamehe tu.” Baada ya kujibu hivyo bwana Kamosa alipigwa busu la ghafla kwenye mdomo na kubaki akitabasamu huku akimwangalia mkewe kwa huba.

Moja kati ya vinyago alivyovipenda sana Dennis,ni hicho cha mwanamke.Laiti kama ukikivutia picha kinyago hicho na kukileta katika mazingira ya kawaida basi ni mwanamke mzuri sana ambaye hakuna kijana angekataa kuwa naye kwa gharama yeyote,ndio maana vijana walikizunguka.

****
Tukirudi katika maisha ya Leonard Kamosa,likizo yake ilikwisha hivyo alirejea kazini.Kamosa aliishi katika mkoa wa Tigalu ulio jirani na mkoa wa Sengeni.Kurudi kwake kazini ni kama alipishana na wafungwa watatu waliotoroka usiku wa jana yake.Taarifa hiyo ilimuumiza kichwa sana kwani walitumia nguvu na muda mwingi sana kuwakamata wafungwa hao wakati huo.

Jinsi Jeshi la Polisi linavyopanga mipango ya kuwakamata wahalifu,ndivyo hivyo hata wahalifu huweka mipango ya kufanya maovu na kuwatoroka Polisi.Pembeni kidogo ya mji mkoani Tigalu,jambazi maarufu kwa jina la Pempre alikuwa akipanga mipango ya kuvamia benki,ilikuwa ni chini ya ardhi kwenye andaki ambalo huwa ni maskani yao.Kilikuwa ni kikundi cha maangamizi.Pempre alimiliki kikundi hicho cha watu saba na kufanikiwa kwa asilimia kubwa kutowesha amani mioyoni mwa raia wa nchi ya Bambai…
Baada ya kuweka mipango sawa,kila mmoja akiwa ndani ya pikipiki yake,waliwasili hapo Benki kwa mwendo wa nusu saa tu.Wateja waliokuwa wakisubiri huduma ndani ya benki waliwekwa chini ya ulinzi ambapo



waliamrishwa kulala kifudifudi.Mama Lisa,mke wa mpelelezi Leonard Kamosa alikuwa ni mmoja kati ya wateja waliowekwa chini ya ulinzi ndani ya benki hiyo.

Baada ya shughuli kukamilika,msala uliibuka.Nje palitapakaa polisi wengi sana huku kila mmoja akiwa ameshika bastora.Basi wale vijana wake walimgeukia Pempre kwa ajili ya kuwapa mpango wa kuwatoroka Polisi
“tufanyaje mkuu?” kijana wake mmoja alihoji
“msijali,ndani ya dakika tano tutakuwa nyumbani tukihesabu pesa.” Alijibu kwa kujiamini Pempre.
Basi wateja ndani ya benki kila mmoja alitokwa na kijasho chembamba kwa uwoga.Pempre alianza kumpitia mteja mmoja baada ya mwingine kwa makini.Alikuwa akiwapiga picha na kutulia sekunde kadhaa kisha kuhamia kwa mwingine.Huku nje Polisi waliendelea kusisitiza kwa kutumia kipaza sauti kwamba Majambazi hao wajisalimishe wenyewe kabla hawajawaingilia ndani.
“mkuu karibu wanaingia!” kijana wake alisisitiza
“usijali,nimefundisha chuo cha polisi kwa miaka sita sasa.” Alijibu pempre kwa kujiamini sana,wakati huo alikuwa amemkaribia Mama Lisa.Alipompiga picha,baada ya sekunde kadhaa alitabasamu na kumwangalia.
“nguo mlizovaa wapeni baadhi ya wateja,kisha ninyi chukueni za kwao.Haraka!” aliamrisha Pempre ambapo vijana wake hawakutumia hata dakika mbili kufanya hilo zoezi.
“tokeni na hao watu,mi nakuja na huyu mke wa Kamosa.” Basi vijana walifanya hivyo ambapo Polisi huku nje waliwakimbilia wale waliovalishwa mavazi ya kijambazi,masikini wa Mungu kumbe walikuwa ni wateja,majambazi walifanikiwa kuondoka isipokuwa Pempre.
“mke wangu bado yupo ndani,” aliongea Leonard kamosa,machozi yakimlenga.Muda huo alikuwa nje ya benki hiyo
“una uhakika?” kiongozi wa msafara alimwuliza Kamosa,kabla hata hajajibu,simu yake iliita.Alikuwa ni mkewe.Kamosa alipokea
“ha ha ha! Kamosaaaa…mke na Pempre yupi bora?” sauti nzito ilisikika hivyo
“naapa kwa mwenyezi Mungu,nitakuua shetani wewe! Mwachie mke wangu.Kama unajiamini onyesha sura yako tupambane kiume.” alijibu kamosa kwa jazba.Pempre kama kawaida yake,hupenda sana kuwasumbua Polisi.Alitoka nje ya benki akiwa amempiga kabali mama Lisa na kumwekea Bastora kichwani.Kamosa kwa jinsi alivyompenda mkewe,alihisi kama bastora



ikifyatuliwa risasi atakufa yeye.Hasira ilimpanda ila alijua vyema Pempre huwa hawazi hata sekunde moja kuua mtu,
“mtu yeyote akiongea au kusogea mahali alipo,huyu mwanamke amekufa.” Alitoa onyo hilo Pempre ambapo kwa mbali mlio mkubwa wa pikipiki ulisikika.Baada ya sekunde kadhaa waliiona pikipiki kwa mbali ikiwa imefunguliwa kasi zote.Polisi wenyewe waliipisha huku wakijifariji na kuachia risasi kadhaa zilizokuwa hazina madhara yeyote.Pikipiki iligeuzia kwa Pempre ambapo Haraka alipanda na kumwacha mama Lisa akitokwa machozi hasa.Polisi walijitahidi kuifukuzia Lakini hawakufanikiwa.

Siku hiyo kwa mama Lisa ilikuwa ngumu sana,si kushuhudia bastora tu,bali kuwekewa kichwani mwake.Ilikuwa ndio mara yake ya kwanza,aliogopa mno,hakuweza kula wala kupata usingizi.Mpaka majira ya saa sita usiku Kamosa alikuwa na kazi ya kumbembeleza mkewe,
“mke wangu,naomba ulale,Mungu amekuokoa kikubwa tumshukuru yeye,” Kamosa alisema hivyo
“usijali mume wangu,nitalala na nitakuwa sawa,ila nikwambie kitu?”
“niambie chochote mke wangu,”
“Pempre ni mwanamke,”
“aah..mke wangu najua…”
“usidhani nimechanganyikiwa mume wangu,nimemsogelea kwa karibu na nimejua,ile sauti nzito ya kiume,kuna kitu amekifunga kwenye shati lake kinabadilisha sauti akiongea,” alimkata kauli na kumwambia hivyo
“sawa mke wangu,naomba tulale kesho tutazungumzia hili.” Kamosa alimsogelea mkewe na kumbusu kisha akamchukua kutoka kwenye kochi la sofa lililopo chumbani humo na kumpeleka kitandani,alimlaza na kumfunika shuka.

***
Pempre alikuwa ni tishio nchini Bambai.Kibaya zaidi kwenye uhalifu alivalia kinyago usoni kilichoficha sura yake mpaka kichwani,ni machoni pekee ndio alipaacha wazi.Aina ya mavazi aliyokuwa akivaa yalimwacha na nafasi kubwa,Kwahiyo hata watu hawakujua Pempre ni wa jinsia gani,kitu pekee kilichowajulisha Pempre ni mwanaume,ni sauti yake nzito.Jambazi huyu hatari alijiamini kupita maelezo kuwa hakuna wa kumzuia kabisa.Kila alilolipanga lilifanikiwa,kukwama hutokea mara chache sana.

Huku upande wa Kamosa,alimpa matumaini mkewe kuwa Suala la Pempre ni mwanamke atalifanyia kazi.ila ndani ya moyo wake alijua wazi kuwa pempre ni mwanaume.Muda huo ilikuwa ni asubuhi,



muda sahihi wa Kamosa kwenda kazini.Basi alitoka nje huku mkewe akimsindikiza kwa utani wa kimahaba.Naweza kusema wawili hawa walipendana sana,wakati huo Lisa alikuwa ndani ya gari akimsubiria baba yake ampeleke shule.Wapendanao hao walipigana mabusu ya kuagana ambapo Kamosa alianza kupiga hatua za taratibu akielekea garini….
Akiwa ameushika mlango wa gari akitaka kuufungua,mkewe alimshtua kwa kumwita jina lake,Kamosa alipogeuza sura yake kumwangalia mkewe,haraka alimfuata.Alipigwa na butwaa pale alipoangalia kilichomshtua kipenzi chake.Tazama…ilikuwa ni picha ya mwanamke ambaye wote walikumbuka walimwona mahali,Kilichoshtua zaidi ni jina la Pempre lilioandikwa chini ya picha hiyo.

Kamosa alipoichukua picha hiyo na kuiangalia kwa karibu,alichanganyikiwa ghafla.Alipoigeuza nyuma,iliandikwa maneno haya…
“naapa kwa mwenyezi Mungu,nitakuua shetani wewe! Mwachie mke wangu.KAMA UNAJIAMINI ONYESHA SURA YAKO TUPAMBANE KIUME.” Ni dhahiri kuwa aliyakumbuka vyema hayo maneno,alimwambia pempre jana yake wakati akiwa amemwekea bastora mkewe kichwani akitishia kumwua kule nje ya Benki jana yake,
“nilikwambia mume wangu,Pempre ni mwanamke,”
“vipi kama anatuchezea akili mke wangu?”
“mi nahisi…alijisikia vibaya ulipomwambia aonyeshe sura yake,jinsi anavyofanya maovu akiwa amejificha sura pengine alijua umemtafsiri,ni mwoga,”
“sawa mke wangu,ila kwanini hii picha ifanane na kile kinyago cha mwanamke kwenye duka la Dennis mkoani Sengeni?”
“hapo ndio mimi nimeshangaa.”

Walimaliza kuongea hivyo ambapo Kamosa aliondoka nayo ile picha kwa ajili ya uchunguzi zaidi.Wakati akielekea ofisini baada ya kumfikisha Lisa shuleni,njiani aliwaza sana kuhusu kile kinyago kufanana na hiyo picha aliyohisi ni ya Pempre.Alibaki akijiuliza maswali kichwani bila kuyapatia majibu
“kama Dennis angejua huyu ni jambazi,kwanini amuweke hadharani?”
“Lakini huwezi kuchonga kinyago cha mtu usiyemjua.” Aliendelea kujiuliza maswali yaliyompelekea kuuona umuhimu wa kwenda kwenye duka la Dennis kufanya mahojiano naye.

Kamosa alipofika ofisini,alipokelewa juu juu na tukio la ushambuliaji lililokuwa likiendelea katika shule aliyokuwa akisoma mwanaye.



Ni dakika chache tu tangu amshushe mwanaye shuleni hapo.Haraka waliwasili kwenye hiyo shule ya mtakatifu Patrick na kukuta hali tofauti.Kamosa alipomwona mwanaye alimkimbilia na kumkumbatia,mpaka machozi yalimtoka.Hakukuwa na majeruhi yeyote wala uharibifu wowote uliofanyika.Ni kama Majambazi walikuja kuitembelea shule hiyo.Watoto walilia kwa uwoga wa kutishiwa bunduki.Kila mwalimu kijasho chembamba kilimtoka kwani walijua ndio siku yao ya mwisho.
“ni mwanamke fulani,alisema anaitwa Pempre,” mwalimu mkuu alitoa maelezo hayo
“alikuwa peke yake?” askari aliendelea kumhoji
“hapana,alikuwa na wanaume wanne wenye pikipiki,”
“baada ya kutoka ofisini ikawaje?”
“alielekea Class five(darasa la tano) kisha baadaye aliondoka.” Askari huyo baada ya kumaliza mahojiano,alishangaa kitu kimoja kwamba Pempre ni mwanamke.Wakati huo bado Kamosa hakuwaonyesha ile picha aliyoikuta nyumbani kwake asubuhi hiyo.

Kamosa baada ya kupewa maelezo na askari aliyekuwa msaidizi wake kwenye shughuli ya upelelezi,alielekea moja kwa moja Class five(darasa la tano) kwa ajili ya kufanya nao mahojiano.Alihitaji kujua nini hasa lilikuwa lengo la Pempre hali ya kuwa hakuiba wala hakuharibu kitu au mtu yeyote.Watoto wa darasa hilo walikusanyika mahali pamoja nje ya darasa ambapo mwanaye pia alikuwa akisoma darasa hilo.
“mwanamke aliyewavamia ndio huyu?” alipaza sauti Kamosa akiwaonyesha ile picha ya Pempre
“ndio.” Walijibu wanafunzi huku wakiogopa isipokuwa Lisa.Kamosa hakushtukia kama mwanaye hakutishwa sana na Pempre
“then she followed Lisa (kisha alimfuata Lisa)” mmoja wa wanafunzi hao alisema.Baada ya kusikia hivyo,Kamosa alipomwangalia mwanaye kwa umakini,ndipo aligundua hayuko kawaida.Taratibu alimfuata na kusogea naye pembeni,waliketi kwenye balaza mbali kidogo na wanafunzi wengine kisha wakaanza kuongea
“Lisa…uliongea na huyu mwanamke?” kwa sauti ya upole alihoji Kamosa.Lisa alitikisa kichwa kuashiria aliongea naye kweli
“mliongea nini?”
“aliniambia amenipenda,na nikifanya vizuri kwenye mtihani wangu wa mwisho atanipa zawadi,”
“hivyo tu?”
“kisha akasema,nisali sana na nisiwe mtu wa kulipiza kisasi,”
“ehee..”

MWISHO






Blog